MAVUNO YA MPUNGA

MREJESHO WA MAVUNO YA KILIMO CHA MPUNGA JATU KWA MSIMU WA MWAKA 2018-2019~KILOMBERO MOROGORO.
——————————————
06.07.2019

UTANGULIZI:
Ndugu wanachama na wakulima wa Mpunga wote mliolima msimu wa mwaka 2018/2019 katika wilaya ya Kilombero chini ya usimamizi wa kampuni ya JATU PLC.

Tunayofuraha kubwa kuwatangazia wastani wa mavuno ya mpunga kwa ekari moja iliyosimamiwa na Jatu katika wilaya ya kilombero.

Kwanza kabisa kabla ya kutoa matokeo napenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo;

 1. Jatu ni kampuni ya Umma ambayo inawaunganisha wanachama na kuwawezesha kulima pamoja kitaalamu kwa kutumia watalaamu ambao ni wafanyakazi wa kampuni ya Jatu.
 2. Mradi wa kilimo cha Mpunga ulianza rasmi mwezi wa kumi mwaka 2018, ambapo jatu iliingia makubaliano ya kusimamia jumla ya ekari 324 za mpunga kwa wanachama wake sabini na mbili (72). Huu ulikuwa ndo msimu wa kwanza kwa kampuni kushiriki mradi wa kilimo cha Mpunga.
 3. Huduma za shamba zote zilifanywa chini ya uongozi wa Meneja msimamizi wa kituo cha Mpunga cha Jatu kilichopo Mbingu, Wilaya ya Kilombero mkoa wa Morogoro.
 4. Wakulima wote walioshiriki mradi huu ni wanahisa wa Jatu na pia ni wanachama wa Jatu Saccos Ltd. wanachama sabini (70) waliomba mkopo na kupewa bila masharti magumu wala riba, lakini wanachama wawili (2) waligharamia gharama zote pasipo msaada wa Jatu Saccos Ltd.
 5. Makadirio ya gharama za mradi huu kwa ekari moja ukitoa gharama za kukodi shamba (Kwa wale waliokodi) na gharama za usimamizi uliofanywa na Jatu, ilikadiriwa kuwa jumla ya tshs. 600,000/- (laki sita) na hivyo mkulima alichangia 1/3 ya laki sita ambayo ni sawa na tshs. 200,000/- ambayo iliwekwa kama akiba Jatu Saccos na kiasi kingine chote mkulima aliomba na kupewa mkopo usio na riba wala dhamana.
 6. Mashamba yaliyolimwa hayakuwa katika eneo moja, mashamba haya yapo katika kata zaidi ya tatu katika wilaya ya kilombero ambazo ni pamoja na Chita, Mgeta na Mbingu. Tuliweza kufanya hivyo, ili kuepuka hasara ambayo inaweza kusababishwa na mafuriko au ukame au magonjwa (wanasema usiweke mayai yote katika kapu moja), ili tuweze kuyajua maeneo mazuri ya kulima mpunga kwa faida ya badae.
 7. Zoezi la kuvuna mpunga lilianza rasmi mwanzoni mwa mwezi June 2019 na kumalizika mwanzoni mwa mwezi July 2019.
 8. Jumla ya gharama zilizotumika kuhudumia ekari moja ni tshs. Laki saba elfu hamsini na nne (754,000/-), ambazo zinajumuisha; gharama ya kulima, haro, mbegu, kupanda, dawa, ng’olezi, mbolea, usafiri, kuvuna na usimamizi wa shamba.
 9. Katika mavuno, mashamba yalitofautiana katika kutoa mazao, kuna baadhi yalitoa mpunga mwingi hadi kufikia gunia 29 kwa ekari moja, na kuna mengine yalitoa mpunga kidogo sana kiasi cha gunia 3 kwa ekari. Lakini wastani wa MAVUNO kwa ekari zote ni GUNIA ISHIRINI NA TATU (23) za DEBE NANE (8) za Mpunga.

CHANGAMOTO
——————————————
Mradi huu umekuwa na changamoto baadhi kutokana na ukweli kwamba ndo mara yetu ya kwanza kusimamia mradi wa mpunga mkubwa kiasi hicho, baadhi ya changamoto tulizokutana nazo ni kama ifuatavyo;

 1. Kuchelewa kuanza kuandaa mashamba na hivyo kupelekea kupishana na msimu kwa wiki kadhaa.
 2. Uhaba wa vitendea kazi kama vile trekta za kulima na mashine za kuvunia.
 3. Mvua kuwa nyingi na kusababisha mafuriko kwa baadhi ya mashamba, mpunga mwingine uliweza kusombwa na maji na hivyo kusababisha baadhi ya maeneo kurudiwa kuoteshwa lakini bado hayakutoa mazao mazuri.
 4. Miundombinu ya usafiri kutokupitika kwa urahisi hasa wakati wa kupanda na kuvuna kutokana na maji kujaa sana kiasi ya kubomoa hata madaraja.
 5. Mabadiliko ya bajeti, kulingana na makadirio yetu ya awali tuliweza kupungukiwa kiasi kidogo kwa ajili ya kukamilisha mahitaji ya shamba eka moja na ukizingatia kwamba tayari mwanachama alishasaini mkopo wake na ni vigumu kumuomba aongeze tena hela kabla ya kuvuna.

TULICHOJIFUNZA/ MABORESHO TUTAKATOFANYA KWA MWAKA UJAO.
——————————————

 1. Tumejiandaa kuanza maandalizi ya mashamba mapema, mwaka jana tulichelewa kuanza na hivyo kupelekea kulima shamba mara moja tu, mwaka huu tutalima mara mbili ili kupunguza ugumu wakati wa ng’olezi.
 2. Tumejiandaa kuongeza vitendea kazi kama vile trekta na combine harvestor kwa ajili ya kuvuna.
 3. Tumejiandaa kutengeneza miundombinu ya usafiri hasa katika yale maeneo ambayo tunayamiliki na tuna mashamba ya kudumu.
 4. Tumejiandaa kuanza kujenga miundombinu ya maji katika mashamba yetu, ili tuweze kuzuia mafuriko lakini pia tuweze kuhifadhi maji kwa ajili ya kulima wakati wa kiangazi.
 5. Kuboresha bajeti yetu msimu ujao, ili tuweze kuepuka changamoto ya kupungukiwa fedha.

MCHANGANUO WA GHARAMA
——————————————
Kabla ya kutoa mchanganuo wa Gharama napenda kuwajulisha kwamba kwa msimu huu tulikuwa na wakulima wa aina mbili, kuna wakulima ambao wanamiliki mashamba yao tayari na kuna wakulima waliokodi mashamba kwa ajili ya kulima msimu mmoja tu. Hivyo basi hapa mchanganuo tunaotoa ni kuanzia kuandaa shamba na ni kwa ekari moja tu kama ifuatavyo;

 1. Kulima (kukatua)~45,000/-
 2. Kupiga Haro~ 30,000/-
 3. Kupanda ~50,000/-
 4. Dawa (round up na 2-4D) ~32,000/-
 5. Mbegu (debe 2) ~22,000/-
 6. Mbolea (CAN + Urea) kg 50 x 2~ 140,000/-
 7. Usafiri wa kupeleka pembejeo shambani ~ 20,000/-
 8. Ulinzi wa ndege na ng’ombe ~ 10,000/-
 9. Kuvuna ~ 217,000/-

Hapa tulitumia njia mbili yaani mashine (combine harvestor) na watu. Kwa kutumia mashine ekari moja iligharimu 150,000/- na kwa kutumia watu ekari moja iligharimu 231,000/- kwa sababu watu hupitia hatua 2; kukata mpunga ekari moja ni 60,000-80,000~ wastani ni 70,000/- na kupiga mpunga ili uweze kupimwa katika viroba ni tshs 7,000/- kwa kila gunia moja, sasa kwa gunia tulizopata 23 ukizidisha 7000 unapata jumla ya tshs. 161,000/- ambayo ukiijumlisha ile 70,000/- ya kukata unapata gharama halisi ya kuvuna ni tshs. 231,000/- na hii ndo gharama iliyotumika kwazaidi ya 75% ya mashamba yetu. Kwa wastani baada ya kujumlisha gharama zote zilizotumika kuvuna tunapata tshs. 217,000/- kama gharama halisi ya kuvuna ekari moja ya gunia 23.

 1. Mifuko ya kuweka mpunga ~23,000/- (1000 x23)
 2. Usafiri wa kutoa mpunga shamba na gharama za kupanga store ~115,000/-
  (Hapa ni sawa 5000 x 23)
 3. Usimamizi wa shamba (JATU)~ 50,000/-

JUMLA KUU: 754,000/-
——————————————

FAIDA TARAJIWA;
Mkulima akiamua kuuza mazao (mpunga) leo kwa bei ya sasa ambayo ni tshs. 7000 kwa debe Sawa na tshs 56,000/- kwa gunia moja la mpunga; atapata jumla ya mauzo ya tshs. 1,288,000/=

Ili kupata faida; toa matumizi yote ambayo ni sawa na 754,000/= utapata faida yako ya sasa ni; 534,000/= Tshs.

Ukizingatia kwamba; wewe ulilipia tu kiasi cha tshs. Laki 2 kama akiba na kupewa mkopo wa kiasi kilichobaki, utakapo amua kuuza mazao yako tutakata gharama zingine zote ambazo wewe hukuzilipia hapo awali.

NENO KUTOKA KWA MKURUGENZI
——————————————
Nawashukuru na kuwapongeza sana wanachama wote mliojitokeza na kushiriki katika mradi huu kwa mara ya kwanza. Mategemeo yetu ilikuwa tupate angalau gunia 30 za mpunga kwa kila ekari moja lakini tumeshindwa kufikia lengo hilo kwa msimu huu. Tunaamini na sasa tumejifunza na kujipanga vizuri, ili kuhakikisha kwamba msimu ujao tunavuka malengo ya gunia 30 kwa kila ekari. Pia tunategemea kuwahudumia wakulima wengi zaidi mwaka huu kwa ekari zaidi ya 1500 ambazo tutazilima kilombero na Kahama. Nawashauri muendelee kuwekeza katika kilimo aidha kwa kununua mashamba au kwa kukodi kwani kimedhihirisha faida nzuri kwa msimu huu. Kwa mfano mwanachama ambaye amelima ekari 50 leo anatengeneza faida ya zaidi ya milioni 20 ndani ya miezi isiyozidi 10. 😊😊 na alichangia milioni 10 tu kama akiba saccoss, ila leo amerudisha gharama zake na faida ya zaidi ya milioni 20 na hakupata usumbufu wa kwenda au kusimamia shamba.

Ni imani yangu kwamba baada ya kutoka kwenye soko la hisa tukaboresha miundombinu yetu vizuri tutaweze kutokomeza umaskini kwa haraka zaidi kupitia kilimo.

MWISHO
————————
Nawashauri wakulima wote mliolima muanze kufatilia mtiririko wa bei ya Mpunga na mchele na ukiona inafaa kuuza fanya maamuzi yako Muda wowote utakao jisikia kwa kuwasiliana na mkuu wa idara ya fedha Jatu PLC ‭+255 65 709 3807‬ utaweza kuuza mazao yako. Lakini pia sio lazima uuze mpunga; unaweza kukoboa mpunga na kuuza mchele. Bei ya mpunga/mchele huwa inaanza kupanda sana kuanzia mwezi October Kwani ndo watu wengi huwa wamemaliza kuvuna, kwa sasa bei iko chini kwa sababu wakulima wengi wamevuna na wanauza mipunga yao kwa wingi. Maana yangu ni kwamba ukisubir bei nzuri utaweza kupata faida hata zaidi ya mara mbili ya faida ya sasa😊.

Asante.
Taarifa hii imetolewa na;
Peter Isare
Mkurugenzi
JATU PUBLIC LIMITED COMPANY.

MATUKIO KWA PICHA YA MSIMU WA MPUNGA 2018/2019