MAVUNO YA MAHARAGE

MREJESHO WA MAVUNO YA KILIMO CHA MAHARAGE JATU KWA MSIMU WA MWAKA 2019~KILINDI, TANGA.

ENEO: KILINDI, TANGA

ZAO: MAHARAGE

MSIMAMIZI: JATU PLC

MMILIKI: MWANACHAMA WA JATU_KILIMO

MUDA: MARCH HADI JULY, 2019

——————————————

UTANGULIZI

Jatu ni kampuni ya Umma ambayo inawaunganisha wakulima na kuwawezesha kulima pamoja kitaalamu kwa kutumia zana za kisasa na watalaamu ambao wamebobea katika kilimo. Jatu inawasaidia wanachama wake katika kutafuta mashamba mazuri, kubuni ni zao gani lilimwe kwa wakati gani, kampuni inahakikisha mashamba yamelimwa na kuandiliwa kitaalamu kabla ya kupanda zao husika, katika kupanda kampuni inahakikisha mbegu sahihi zimetumika, huduma ya mmea kwa kila hatua ndo jukumu kuu la kampuni ya JATU. Ni wajibu wa JATU kuhakikisha mteja anapata soko la uhakika kwa mazao yote ambayo amelima.

Mwanzoni mwa mwaka huu, wataalamu wa jatu walianza kufanya utafiti wa kilimo cha maharage katika mkoa wa Tanga, lengo ilikuwa ni kujua ni eneo gani zao hili linaweza kulimwa na kustawi pasipo kutegemea umwagiliji, pia wataalamu wetu walilenga kupata eneo ambalo lina ardhi kubwa na ambayo inapatikana kwa gharama nafuu kwa kukodi na hata kwa kununua. Katika utafiti huu tuligundua kwamba Wilaya ya kilindi ni sehemu sahihi kwa kilimo hichi cha maharage.

Kilindi ni wilaya ndani ya Mkoa wa Tanga. Imepakana na wilaya ya Kiteto mkoa wa Manyara, pia imepakana na wilaya ya Handeni kwa upande wa mashariki, mkoa wa Kilimanjaro upande wa Magharibi-kaskazin, na mkoa wa Morogoro upande wa kusini. Wilaya ya kilindi ina jumla ya kata 21 na vijiji 102 ambavyo vyote vina ardhi nzuri ya kilimo. Ni eneo la milima milima yenye rotuba. Kuna mvua za kutosha katika eneo hili, mazao yanayokubali katika ardhi ya Kilindi ni pamoja na Maharage, Mahindi na Alizeti.

KWA NINI JATU TUMEAMUA KUANZA KILIMO CHA MAHARAGE?

Zao la Maharage ni muhimu katika mfumo wa JATU kwa sababu kuu zifuatazo;

 1. Maharage ni lishe ya pili kwa umuhimu Nchini Tanzania baada ya mahindi.
 2. Jatu inajihuzisha na kuuza chakula kwa wanachama wake kwa lengo la kujenga afya. Ili ujenge afya unahitaji kula chakula chenye virutubitsho na madini muhimu kwa ukuaji wako, na mahargae ni moja ya chakula ambacho kina protini nyingi. Protini ni muhimu sana katika kujenga mwili na kuwezesha ukuaji wa mwili hasa kwa watoto na pia husaidia kutengeneza kinga ya mwili.
 3. JATU tunalima alizeti, mahindi na mpunga, maharage yanatumika kama mboga kwa familia nyingi ambazo zinanua unga kwetu au mafuta ya kula ya alizeti.
 4. Tunazalisha na kuuza mchele, familia nyingi zinatumia maharage hasa wanapokuwa wamepika wali. Hivyo ni vyema na muhimu kuwa na maharage katika mfumo wa JATU ili mteja wetu aweze kupata bidhaa zote kwa mara moja sehemu moja na apate kilicho bora kwa gharama nafuu.

MCHAKATO WA KILIMO ULIVYOANZA KWA ZAO HILI LA MAHARAGE

Mwaka huu mwezi wa tatu ndo tumeanza kulima maharage kwa mara ya kwanza, tulianza kama majaribio ili kujua uhalisia wa zao hili kwa vitendo, huu ulikuwa ni mwendelezo wa utafiti wetu katika zao hili kabla hatujajikita rasmi katika hichi kilimo. Na kwa sababu hii, mashamba ambayo tulilima msimu huu yalikuwa ya kukodi, jumla ya ekari mia mbili arobaini na saba (247) zimelimwa msimu huu, Mashamba yetu tuliyapata vijiji vitatu tofauti vya eneo la kibirashi, ni ngumu sana kupata ekari zote 247 kwa sehemu moja na hivyo tulilazimika kutafuta kidogo kidogo na tulibahatika kupata kati ya ekari 40-60 kwa eneo moja.

WASHIRIKI WA MRADI HUU

Wakulima wote walioshiriki mradi huu ni wanachama wa Jatu na pia ni wanachama wa JATU SACCOS LTD. Wanachama 77 waliweza kukodi jumla ya ekari 247 kwa ajili ya kulima maharage.

MFADHILI WA MRADI HUU

Mradi huu ulihuzisha watu wa aina tatu kama ifuatavyo:

 1. MKULIMA
 2. JATU SACCOS LIMITED
 3. JATU PUBLIC LIMITED COMPANY

MKULIMA alifadhili mradi huu akiwa kama mmiliki wa mradi yeye alikodi shamba na akachangia 1/3 ya gharama zote za kilimo (hizi gharama hazijumuishi gharama za kuvuna). Na pia mkulima alitoa nusu ya gharama za kuvuna.

JATU SACCOS LTD ilitoa mkopo wa kilimo kwa wakulima wote bila Riba, mkopo huu ni 2/3 ya gharama zote za kilimo (mkopo huu haukuhuzisha sehemu ya mavuno).

JATU PLC ilitoa nusu ya gharama za kuvuna kwa mkulima kwa makubaliano kwamba mkulima atamrudishia gharama hizo mara baada ya mavuno.

MCHANGANUO WA GHARAMA ZILIZOTUMIKA KWA EKARI 1

 1. Kulima round 1; 30,000/-
 2. Kulima round 2; 25,000/-
 3. Mbegu (Njano); 6000/-x30kg=180,000/-
 4. Kupanda; 32,000/-
 5. Mbolea ya kupandia (DAP); 1500/-x24kg = 36,000/-
 6. Kuweka mbolea; 10,000/-
 7. Dawa ya kuzuia wadudu DVA -Profit EC 720 na DUDUBA EC 450; 45,000 + 25,00 = 70,000/=
 8. Kupiga dawa; 10,000/-
 9. Kupalilia palizi 2; 60,000/-
 10. Walinzi wa shamba; 5,000/-

JUMLA YA GHARAMA; 458,000/-

GHARAMA ZA KUVUNA kwa GUNIA

 1. Kung’oa na kumenya; 15,000/-
 2. Kuchambua na kusafisha; 15,000/-
 3. Mifuko ya kufungia; 1,000/-
 4. Usafiri kutoka shamba hadi store/sokoni; 10,000/-

JUMLA YA GHARAMA ZA GUNIA MOJA; 41,000/-

Kwa gunia 14 ni sawa na tshs. 574,000/-

USIMAMIZI

1. Gharama za kulipa wataalamu; 50,000/-

2. Gharama za usafiri wa zana za kilimo kama vile mbegu, mbolea n.k; 36,000/-

JUMLA; 86,000/- kwa EKARI 1

JUMLA YA GHARAMA ZOTE ZILIZOTUMIKA KWA EKARI MOJA NI;

1,118,000/-

MAVUNO

Zoez la kuvuna lilianza tarehe 21st July, 2019 na kukamilika tarehe 29th July, 2019. Mavuno yetu tuliweza kuyapima katika magunia ya kilogram 100 baada ya kumaliza mavuno; jumla ya magunia yaliyopatikana kwa ekari zote 247 ni 3,458. Wastani wa kila ekari hapa ni sawa na gunia 14 hizi ni sawa na kg 1,400 kwa kila ekari Moja.

SOKO LA HAYA MAZAO NA BEI TARAJIWA

Kwa kuwa JATU inahitaji maharage kwa ajili ya soko lake ambalo ni wanachama, na kwamba jatu aliahidi kununua mazao ya wakulima mara ya baada ya kuvuna, basi maharage yote ambayo yamevunwa mwaka huu yatanunuliwa na kampuni ya JATU PLC kwa bei ya soko na kwa muda ambao mkulima atahitaji kuuza mazao yake. Bei itakayotumika na bei ya wilaya ya kilindi ambako ndipo maharage yalipolimwa.

FAIDA TARAJIWA KWA MKULIMA

Bei ya maharage ndio inaweza kuonesha faida ambayo mkulima anaweza kuipata baada ya kuuza na kutoa gharama zake. Kwa sasa bei ya maharage ipo chini ukilinganisha na bei ya kuanzia mwezi wa October, hii inasababishwa na ukweli kwamba sahizi ni muda wa mavuno na  wakulima wengi wanauza maharage hivyo kupelekea bei kuwa chini. Hata hivyo bei ya sasa ni kati ya 1500-1800 kwa kilo moja ya maharage.

Angalia mfano wa kielelezo kifuatacho kujua makadirio

Kielelezo;

Kwa mfano; mkulima akiuza kwa bei ya Tshs. 1800 kwa kg leo mchanganuo wa faida yake itakuwa kama ifuatavyo:

ZAO EKARI BEI (TSHS) KIPIMO KG JUMLA YA KG MAUZO TSHS GHARAMA TSHS FAIDA TSHS
MAHARAGE 1 1800 1KG   1400 2,520,000 1,118,000 1,402,000

CHANGAMOTO

——————————————

Mradi huu umekuwa na changamoto baadhi kwa sababu ni mara ya kwanza kulima zao hili katika wilaya hii ya kilindi. Baadhi ya changamoto tulizokutana nazo ni kama ifuatavyo;

 1. Kuchelewa kuanza kuandaa mashamba na hivyo kupelekea kupishana na msimu kwa wiki kadhaa.
 2. Uhaba wa vitendea kazi kama vile mashine za kupandia, palizi, kupiga dawa na kuvunia. Tumetumia nguvu kazi ya binadamu kwa Zaidi ya asilimia 75 ya mradi huu na hivyo kupelekea kupata changamoto ya muda na ufanisi.
 3. Mabadiliko ya bajeti, kulingana na makadirio yetu ya awali tuliweza kupungukiwa kiasi kidogo kwa ajili ya kukamilisha mahitaji ya shamba hasa kwa hatua za awali kabla ya mavuno.
 4. Wadudu, kwa mwaka huu eneo la kilindi liliweza kushambuliwa na wadudu na zao la maharage liliadhiriwa kwa sehemu, hii pia ilipelekea bajeti yetu ya dawa kuathiriwa kwa sehemu kubwa sana ukilinganisha na makadirion tuliyokuwa tumeweka awali.
 5. Jua, mvua yam waka huu haikuja kama ilivyokuwa imezoeleka kwa eneo hili na hivyo majira ya kupanda yalipishana na majira ya mvua, hili lilipelekea mimea kukosa maji ya kutosha kwa wakti sahihi.

MABORESHO TUTAKAYOFANYA KWA MWAKA UJAO.

——————————————

 1. Tumejiandaa kuanza maandalizi ya mashamba mapema ili kuendana na msimu wa mvua kwani mvua.
 2. Tumejiandaa kuongeza vitendea kazi kama vile trekta za kulima, mashine ya kupandia, mashine za kupalilia, mashine za kupigia dawa pamoja na mashine za kisasa za kuvunia maharage.
 3. Tuwe na mashamba ya kudumu na tuepukane na mashamba ya kukodi.
 4. Tuanze mkakati wa kuchimba au kuvuna maji ili tuweze kulima kilimo cha kisasa cha umwagiliaji.
 5. Kuboresha bajeti yetu msimu ujao, ili tuweze kuepuka changamoto ya kupungukiwa fedha.

UJENZI WA KITUO CHA KUDUMU CHA KUCHAMBUA NA KUFUNGASHA MAHARAGE KATIKA WILAYA YA KILINDI, TANGA

Kulingana na umuhimu wa zao hili la kilimo cha maharage katika wilaya ya kilindi kampuni ya Jatu imeamua kujenga kituo cha kudumu ambapo kituo hichi kitakuwa na kazi zifuatazo:

 1. Kuhifadhi maharage
 2. Kuchambua na kusafisha maharage
 3. Ofisi ya wataalamu wa kilimo na umwagiliaji
 4. Kuhifadhi vifaa vya kilimo
 5. Kununua maharage kutoka kwa wakulima

NENO KUTOKA KWA MKURUGENZI

——————————————

Nawashukuru na kuwapongeza sana wanachama wote mliojitokeza na kushiriki katika mradi huu kwa mara ya kwanza. Mategemeo yetu ilikuwa tupate angalau gunia 20 za Maharage kwa kila ekari moja lakini tumeshindwa kufikia lengo hilo kwa msimu huu.

Tunaamini na sasa tumejifunza na kujipanga vizuri, ili kuhakikisha kwamba msimu ujao tunavuka malengo ya gunia 20 kwa kila ekari. Pia tunategemea kuwahudumia wakulima wengi zaidi mwaka huu kwa ekari zaidi ya 1000 ambazo tutazilima kilindi.

Nawashauri muendelee kuwekeza katika kilimo kwa kununua mashamba kwani kimedhihirisha faida nzuri kwa msimu huu. Kwa mfano mwanachama ambaye amelima ekari 20 leo anatengeneza faida ya zaidi ya milioni 30 ndani ya miezi isiyozidi minne (4), bila usumbufu wa aina yeyote hasa wa kusimamia mashamba.

Ni imani yangu kwamba baada ya kutoka kwenye soko la hisa tukaboresha miundombinu yetu vizuri tutaweze kutokomeza umaskini kwa haraka zaidi kupitia kilimo.

MWISHO

————————

Nawashauri wakulima wote mliolima muanze kufatilia mtiririko wa bei ya Maharagea na ukiona inafaa kuuza fanya maamuzi yako Muda wowote utakao jisikia kwa kuwasiliana na mkuu wa idara ya fedha Jatu PLC +255 65 709 3807 utaweza kuuza mazao yako.

Asante.

Taarifa hii imetolewa na;

Peter Isare

Mkurugenzi

JATU PUBLIC LIMITED COMPANY.

PICHA ZA HATUA MBALIMBALI ZA MRADI