HABARI

JATU PLC KUSHIRIKI KATIKA MAONYESHOYA 5 YA BIDHAA ZA VIWANDA

Kampuni ya JATU PLC ni miongoni mwa makampuni yanayoshiriki katika maonesho ya tano(5) ya bidhaa za viwanda yaliyoanza rasmi tarehe 3-9 Desemba 2020 chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia tasisi yake ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya Tanzania (TanTrade).

Maonesho haya ambayo yanafanyika katika Viwanja vya maonesho ya Sabasaba wilayani Temeke yanalenga kutambua mchango wa viwanda nchini na kujenga jukwaa kwa wadau wa sekta ya viwanda kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na kutangaza fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.

Kupitia maonesho haya, JATU PLC inapenda kuwakaribisha Watanzania wote kushiriki katika maoenesho haya na kuweza kujifunza fursa mbalimbali ndani ya JATU ikiwemo uuzwaji wa bidhaa za JATU zinazochakatwa katika viwanda vya JATU ikiwemo bidhaa za chakula kama maharage, mchele, unga wa lishe, sembe na dona, mafuta ya kupikia nk, shughuli ambayo inamuhakikishia mteja bidhaa ambazo zitamjengea afya bora na kumuongezea kipato kwa kupata gawio la faida kila mwisho kutokana na manunuzi ya bidhaa za JATU.

Akizungumza hivi karibuni katika maonesho hayo Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Bi. Latifa Khamis amesema, “maonesho haya yanahamasisha Watanzania kutumia bidhaa zao kama kauli mbiu inavyosema, ‘Tumia bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania’‘, alisema Bi. LATIFA.

JATU PLC YAINGIA DSE KWA KISHINDO

Imeelezwa kuwa utendaji na uongozi madhubuti wa Rais Dkt. John Joseph Magufuli katika kuweka mikakati na mazingira wezeshi, shirikishi na endelevu kisera imechochea ukuaji wa sekta ya fedha hususani katika masoko ya mitaji na uchumi kwa ujumla nchini.

Hayo yameelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Nicodemus Mkama jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa hisa za JATU Plc katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE.) “Nawashukuru wadau wa sekta ya fedha kwa kuhudhuria hafla hii ya kuorodheshwa kwa hisa za Kampuni ya JATU Plc kwenye soko la hisa la Dar es Salaam, huu ni uthibitisho kwamba sekta ya fedha ina wadau wengi wanaounga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli iliyoweka mazingira wezeshi na kiutendaji yenye malengo ya kukuza uwekezaji kupitia masoko ya mitaji.” Ameeleza.

Amesema kuwa, hisa zapatazo 2,164,349 kutoka Kampuni ya JATU Plc zimeorodheshwa katika soko la hisa na hiyo ni kutokana na matokeo chanya ya elimu na ufahamu walioupata viongozi waanzilishi wa JATU Plc ambao ni vijana wa kitanzania waliotumia fursa hiyo baada ya kushiriki shindano la masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini. Pia ameipongeza JATU Plc kwa kujidhatiti kwa kuwekeza katika sekta mbalimbali pamoja na kutoa ajira zipatazo 10,650 wakiwemo wanawake kwa asilimia kubwa na kuwahimiza kuendelea kufanya kazi kwa uaminifu ili kuweza kufikia azma ya maendeleo.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Moremi Marwa amesema, Kampuni ya JATU Plc imeorodhesha hisa zake 2,164, 349 zenye ukubwa wa mtaji wa thamani ya shilingi Bilioni moja na Milioni 83. Amesema, malengo kwa kuorodhesha hisa za JATU ni kuwezesha wanahisa wa JATU Plc kuendelea kununua na kuuza hisa zao katika bei inayoamuliwa na soko. “Ninaupongeza uongozi wa JATU kwa kufikia hatua hii na kuwapa imani wana hisa wake kupitia shughuli wanazozifanya ikiwemo kilimo na masoko, hii ni hatua kubwa katika kuelekea maendeleo. Tunaamini kupitia hatua hii ajira zitazalishwa kwa wingi pamoja na kuongeza pato la Serikali kupitia kodi.” Ameeleza.

Mkurugenzi Mtendaji wa JATU Plc Ndg. Peter Isare, alisema kampuni hiyo inayomilikiwa na wanawake, vijana pamoja na watu wa kipato cha kati, wamejiunga pamoja na kushirikiana katika miradi mikubwa ya kilimo, viwanda, masoko na Tehama. Hadi kufikia mafanikio hayo ya kusajiliwa soko la hisa, wameweza kuanzisha mashamba katika hekari zipatazo 17,678 yaliyopo katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo Tanga, Manyara, Singida, Ruvuma, Morogoro na Njombe. Hatua ya kampuni kuorodheshwa katika soko la hisa kutazidi kuiwezesha kushiriki katika miradi mikubwa zaidi na hivyo kuisaidia kubadilisha maisha ya maelfu ya watanzania.


Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama akipiga kengele kuashiria kufunguliwa kuanza kuuzwa kwa hisa za kampuni ya JATU PLC katika Soko la Hisa la Dar Es Salaa (DSE), kwenye hafla fupi ya kuorodheshwa kwa hisa za Kampuni ya JATU Plc katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE).

HATIMAYE JATU PLC KUINGIA KATIKA SOKO LA HISA (DSE).

Ikiwa ni mwaka wa nne tangu kuanzishwa kwa kampuni ya JATU PLC, mnamo tarehe 14.11.2020 kampuni ya JATU PLC iliitisha mkutano mkubwa katika ukumbi wa Blue Pearl Hotel, Ubungo Plaza, iliyokutanisha bodi ya wakurugenzi wa JATU PLC pamoja na wanachama wa kampuni. Ajenda kuu ikiwa ni mchakato wa kampuni ya JATU PLC kuingia katika soko la HISA. Aidha ajenda mbalimbali zilijadiliwa katika mkutano huo, ikiwemo uwasilishaji wa ripoti ya mwaka na taarifa za fedha, kupitisha na kuzindua miradi mipya ya kilimo kwa mazao ya mboga mboga, kitunguu na viazi lishe pamoja na kuzindua fursa ya uwakala wa bidhaa za Jatu

Mkurugenzi wa JATU PLC Ndg. Peter Isare Gasaya ameshauri watanzania kutambua fursa zitolewazo na kampuni sambamba na kujiunga ili kuweza kushiriki katika fursa na miradi mbalimbali inayoendeshwa na kampuni kupitia umiliki wa hisa za kampuni. Aidha aliendelea kueleza kuwa baada ya kuingia katika soko la hisa kuanzia mwaka huu 2020 kampuni inategemea mahitaji makubwa ya bidhaa kuongezeka, wawekezaji hususani kwenye miradi ya kilimo kuongezeka na hivyo kufikia dhima ya kampuni ya kuhakikisha upatikanaji wa chakula bora katika ukanda wa Afrika Mashariki sambamba nakutokomeza umasikini.

Aliendelea, “Kilimo kwa tafsiri ya JATU ndio nguzo na mustakabali wa kujenga kampuni ya JATU kwa kupitia matokeo ya mwisho ya kufanikisha ‘KULA ULIPWE’. tukifanikiwa kuwa na mazao mengi, viwanda na bidhaa na uwepo wa mawakala wengi tutahakikisha ufikiaji wa bidhaa za JATU kwa kila mtu”. Pia Ndg. Peter Isare aliwataka watanzania kuona fursa katika kilimo cha zao la parachichi ili kunufaika na soko la kimataifa.

Naye Mwenyekiti wa bodi wa JATU PLC Mhandisi Dk.Zaipuna Yona alisisitiza na kutoa wito kwa vijana kuondokana na fikra za kudhani ni wazee ndio wanatakiwa kujihusisha na masuala ya uwekezaji katika masoko ya hisa na kuwataka wajifunze zaidi katika faida za uwekezaji kupitia masoko ya hisa. Aidha Dk. Zaipuna aliendelea kuelezea faida mbalimbali za kujiunga na kampuni ya JATU PLC zikiwemo kupata usimamizi wa kitaalamu katika shughuli za kilimo, uwezeshwaji wa mikopo isiyo na riba, faida ya kupata gawio la faida kutokana na manunuzi ya bidhaa za chakula zinazouzwa na kampuni ya JATU. nk.

KUELEKEA MKUTANO MKUU WA WANAHISA TAREHE 14.11.2020

Ikiwa zimebaki siku chache, kampuni ya JATU PLC inapenda kuwataarifu wanachama wa JATU na wote ambao bado hawajajisajili kuwa wanachama juu ya mkutano mkubwa wa wanahisa unaotarajia kufanyika siku ya Jumamosi ya tarehe 14.11.2020.

WALENGWA

  • Wanahisa wa JATU PLC.
  • Wanachama wa JATU.
  • Wageni ambao si wanachama wa JATU na wangependa kufahamu fursa zinazopatikana ndani ya JATU.

AJENDA

  • Mrejesho kuhusu mchakato wa kampuni kuingia katika soko la hisa.
  • Uzinduzi wa fursa ya Uwakala wa uuzaji na usambazaji wa bidhaa za JATU.
  • Uzinduzi wa miradi mipya ya kilimo kwa mazao ya VIAZI LISHE na VITUNGUU.

JINSI YA KUSHIRIKI

  • Washiriki wote wanaotarajia kushiriki katika mkutano huu wanatakiwa kuwa na fulana – (T-shirt) ya JATU inayopatikana katika mfumo wa JATU MARKET au kwa kufika katika ofisi za Makao Makuu ya JATU zilizoko Posta, mtaa wa Samora katika jengo la PSSSF HOUSE ghorofa namba 6.

MUDA

  • Kuanzia saa 02:00 Asubuh mpaka 11:00 Jioni

JATU NI YA KWETU

WOTE MNAKARIBISHWA

TANGAZO MUHIMU KWA WAKULIMA WALIONUNUA MASHAMBA YA JATU KITETO, ENDELEA KUFUATILIA BLOG YETU KWA TAARIFA ZAIDI

Tunapenda kuwataarifu wanachama wakulima walionunua mashamba wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara, kwamba kutakuwa na kikao kitachofanyika ofisi za Posta Jengo la PSSSF, ghorofa namba 11 ukumbi wa mikutano kuanzia saa 03:00 asubuhi hadi saa 05:00 asubuhi, tarehe 19 septemba, 2020.

Agenda kuu ni utoaji wa hati miliki za mashamba kwa awamu ya kwanza, hii inawahusu wale tu, waliosafisha na kung’oa visiki pamoja na walionunua mashamba safi lakini pia walioshiriki mchakato wa kugharamia gharama za kuingia soko la hisa (DSE).

Pakua tangazo la wakulima walionunua mashamba Kiteto

MAANDALIZI YA KILIMO CHA PARACHICHI NA JATU NJOMBE YAZIDI KUSHIKA KASI, ENDELEA KUFUATILIA BLOG YETU KWA TAARIFA ZAIDI

Ikiwa ni takribani wiki mbili tangu sikukuu ya wakulima(Nanenane day) iliofanyika tarehe 08/08/2020 pale Ubungo Plaza Dar es salaam, tukio lililohudhuriwa na watu zaidi ya mia saba likiambatana na uzinduzi rasmi kwa mradi wa kilimo cha parachichi unaofanyika mkoani Njombe ambapo mpaka sasa maandalizi yake yameshika kasi baada ya timu ya JATU TV ikiongozwa na Mkurugenzi wa JATU PLC Ndg. Peter Isare kutembelea eneo hilo kujionea kinachoendelea.

Akiongea na JATU TV Mkurugenzi wa JATU PLC Ndg. Peter Isare amesema, “Tupo katika shamba letu ambalo tayari tumeshaanza mchakato wa kuandaa mazingira kwaajili ya kilimo cha kisasa cha parachichi hapa Njombe mpakani kabisa na Mlimba na kama mnavyoona tayari kazi inafanyika na maandalizi ya shamba tayari yameshafanyika. Kwahiyo sasa hivi tumeshamaliza hatua ya kwanza ambayo ni kufyeka shamba na sasa tunaendelea na taratibu zingine za maandalizi, na tunategemea ifikapo mwezi disemba mwaka huu tayari tutakua tunaelekea hatua ya ya pili ambayo sasa ni kuingiza mazao yetu shambani. Pia napenda kutoa wito kwa wanachama na wasio wanachama wa JATU ambao wangependa kujiunga na mradi huu kuwa hatua ya kwanza inakaribia kufungwa hivyo wachangamkie fursa mapema kabla muda haujawapita”

Pia JATU TV ilifanya mazungumzo na mtaalamu wa kilimo anaesimamia mradi huu wa parachichi Ndg. Ditto Francis na kusema, “Tayari tumeshaweka vitalu kwaajili ya kuzalisha miche ya parachichi, vitalu vinaendelea vizuri na tunaendelea kuvimwagilia vizuri, tumevitengenezea mazingira ya kitaalamu ya kuhakikisha miche mizuri na yenye afya inatoka ambayo tutayoitumia kwenye shamba letu ambalo mpaka januari mwakani tutalianzisha rasmi. Vitalu vyetu tumevielekeza karibu na mto ambapo kuna maji ya kutosha ili iwe rahisi kwa zoezi la umwagiliaji”.

WANANCHI ZAIDI YA 100 WASHIRIKI KATIKA SEMINA YA JATU PLC, ENDELEA KUFUATILIA BLOG YETU KWA TAARIFA ZAIDI

Kampuni ya JATU PLC siku ya Jumamosi ya tarehe 22 Agosti 2020, ilitoa fursa kwa wakazi wote ndani ya jiji la Dar es Salaam kuweza kushiriki katika semina maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kiujasiriamali na uwekezaji.

Semina hizi zina lengo la kutoa mafunzo ya fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya JATU PLC ikiwemo uwekezaji kupitia kilimo, viwanda, fursa katika biashara ya mazao, namna mwanachama wa JATU anavyoweza kujiongezea kipato kupitia masoko ya bidhaa za chakula za JATU, uwezeshwaji kupitia mikopo yenye masharti nafuu na namna mtu mwenye mawazo chanya ya kimaendeleo anavyoweza kuwezeshwa kwa mtaji ili kuweka wazo lako katika vitendo kupitia program mpya ya JATU TALK.

Aidha, semina hizi zitakuwa zikifanyika siku za Jumamosi katika kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya fursa zinazopatikana JATU zinazoweza kumkomboa mmoja kutoka katika umaskini na kumjengea afya bora kama ilivyo dhima ya kampuni ya JATU.

Tunatoa wito kwa Watanzania wote kuweza kushiriki katika semina hizi za JATU zinazofanyika siku za Jumamosi katika ofisi za JATU zilizoko Posta, jengo la PSSSF House ghorofa ya 11 ili kufahamu fursa lukuki zenye kuleta maendeleo.

Asante na karibu

JATU-Jenga Afya Tokomeza Umaskini

SEMINA ZA JATU ZA KILA JUMAMOSI ZIMERUDI TENA, ENDELEA KUFUATILIA BLOG YETU KWA TAARIFA ZAIDI

Baada ya kusubiri kwa muda mrefu sasa semina za kila Jumamosi zinazoandaliwa na JATU zimerudi tena. Usikose kuhudhuria semina itakayofanyika Jumamosi ya tarehe 22.08.2020 (kesho) kufahamu fursa wakadha ndani ya JATU.

Lengo la semina hizi ni kufungua fursa za uwekezaji kwenye kilimo, viwanda, masoko na mikopo ambazo zinapatikana kupitia JATU PLC ili kutimiza azma ya kujenga afya na kutokomeza umasikini kwa watanzania wote.

USIPITWE NA MAVUNO EXTRA NA JATU PLC, TUKUTANE SOKONI

FURSA KWA WANUNUZI WA MAZAO NA JATU

Ni muda wa mavuno extra sasa mazao yote yapo sokoni kwa wadau ambao wangependa kununua mazao ya wakulima wa JATU yaliohifadhiwa kwenye maghala yetu kwa bei ya soko kipindi hiki cha mavuno kupitia JATU market App na kisha kuyauza baadae bei za soko zikipanda kupitia viwanda vyetu wanakaribishwa kufanya biashara na wakulima wetu. Lengo la JATU ni kuongeza wigo na faida ya kilimo biashara huku tukitimiza azma yetu ya kujenga afya na kutokomeza umasikini.

Ni muda wa Mavuno Extra Tukutane Sokoni