JATU PLC YAINGIA DSE KWA KISHINDO

Imeelezwa kuwa utendaji na uongozi madhubuti wa Rais Dkt. John Joseph Magufuli katika kuweka mikakati na mazingira wezeshi, shirikishi na endelevu kisera imechochea ukuaji wa sekta ya fedha hususani katika masoko ya mitaji na uchumi kwa ujumla nchini.

Hayo yameelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Nicodemus Mkama jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa hisa za JATU Plc katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE.) “Nawashukuru wadau wa sekta ya fedha kwa kuhudhuria hafla hii ya kuorodheshwa kwa hisa za Kampuni ya JATU Plc kwenye soko la hisa la Dar es Salaam, huu ni uthibitisho kwamba sekta ya fedha ina wadau wengi wanaounga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli iliyoweka mazingira wezeshi na kiutendaji yenye malengo ya kukuza uwekezaji kupitia masoko ya mitaji.” Ameeleza.

Amesema kuwa, hisa zapatazo 2,164,349 kutoka Kampuni ya JATU Plc zimeorodheshwa katika soko la hisa na hiyo ni kutokana na matokeo chanya ya elimu na ufahamu walioupata viongozi waanzilishi wa JATU Plc ambao ni vijana wa kitanzania waliotumia fursa hiyo baada ya kushiriki shindano la masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini. Pia ameipongeza JATU Plc kwa kujidhatiti kwa kuwekeza katika sekta mbalimbali pamoja na kutoa ajira zipatazo 10,650 wakiwemo wanawake kwa asilimia kubwa na kuwahimiza kuendelea kufanya kazi kwa uaminifu ili kuweza kufikia azma ya maendeleo.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Moremi Marwa amesema, Kampuni ya JATU Plc imeorodhesha hisa zake 2,164, 349 zenye ukubwa wa mtaji wa thamani ya shilingi Bilioni moja na Milioni 83. Amesema, malengo kwa kuorodhesha hisa za JATU ni kuwezesha wanahisa wa JATU Plc kuendelea kununua na kuuza hisa zao katika bei inayoamuliwa na soko. “Ninaupongeza uongozi wa JATU kwa kufikia hatua hii na kuwapa imani wana hisa wake kupitia shughuli wanazozifanya ikiwemo kilimo na masoko, hii ni hatua kubwa katika kuelekea maendeleo. Tunaamini kupitia hatua hii ajira zitazalishwa kwa wingi pamoja na kuongeza pato la Serikali kupitia kodi.” Ameeleza.

Mkurugenzi Mtendaji wa JATU Plc Ndg. Peter Isare, alisema kampuni hiyo inayomilikiwa na wanawake, vijana pamoja na watu wa kipato cha kati, wamejiunga pamoja na kushirikiana katika miradi mikubwa ya kilimo, viwanda, masoko na Tehama. Hadi kufikia mafanikio hayo ya kusajiliwa soko la hisa, wameweza kuanzisha mashamba katika hekari zipatazo 17,678 yaliyopo katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo Tanga, Manyara, Singida, Ruvuma, Morogoro na Njombe. Hatua ya kampuni kuorodheshwa katika soko la hisa kutazidi kuiwezesha kushiriki katika miradi mikubwa zaidi na hivyo kuisaidia kubadilisha maisha ya maelfu ya watanzania.


Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama akipiga kengele kuashiria kufunguliwa kuanza kuuzwa kwa hisa za kampuni ya JATU PLC katika Soko la Hisa la Dar Es Salaa (DSE), kwenye hafla fupi ya kuorodheshwa kwa hisa za Kampuni ya JATU Plc katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE).

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s