FAHAMU KUHUSU KILIMO CHA PARACHICHI NA JATU MKOANI NJOMBE, PAKUA JATU TALK APP KUPATA TAARIFA ZA MRADI HUU

Download nakala ya mradi wa kilimo cha Parachichi na JATU

SEHEMU YA KWANZA

Parachichi ni zao linalooteshwa katika ukanda wa baridi na katika ardhi yenye rotuba na maji ya kutosha. Njombe, Iringa, Mbeya, Morogoro, Tanga na Kilimanjaro ni baadhi tu ya mikoa inayolima Parachichi kwa wingi hapa Tanzania.

Jatu tumechagua kulima Parachichi katika mkoa wa Njombe, wakati tunatafuta mashamba tulizunguka maeneo mbali mbali ya mkoa wa Njombe na ni kweli mashamba yanapatikana maeneo mengi tu katika mkoa huu. Baada ya kutembelea maeneo hayo tuliamua kuchukua mashamba yaliyopo Njombe vijijini katika Eneo la madeke. Madeke ambako tumepata shamba ni mpakani kabisa mwa Njombe na Morogoro. Upande wa pili wa Morogoro tumetenganishwa na mto mkubwa wa kudumu unaitwa MFUJI na mashamba yetu yapo upande wa Njombe na upande wa Morogoro pia. Upande wa Njombe ni kijiji cha madeke, kata ya Lupembe. Na upande wa Morogoro ni kijiji cha Taweta, kata ya masagati halmashauri mpya ya Mlimba.

This image has an empty alt attribute; its file name is hass-avocado-4131531_1920.jpg

Hili eneo tumelichagua kuwekeza kwa sababu; kwanza kuna ardhi kubwa yenye rotuba, Kuna maji ya uhakika, kuna uwanda mzuri Yaani milima sio mikubwa sana ukilinganisha na maeneo mengine ya mkoa wa Njombe, barabara inapitika na shamba liko barabarani pia kuna reli ya Tazara inapita karibu na hili shamba upande wa mlimba, miundombinu ya umeme ipo Karibu na shamba, hali ya hewa inaruhusu kilimo cha Parachichi.

Gharama ya shamba katika eneo hili ni kati ya 250,000 – 500,000 likiwa na asili ya msitu. Bei zinatofautiana na zinabadilika kutokana na maamuzi ya muuzaji maana mashamba yanamilikiwa na watu tofauti tofauti hivyo kila mmoja ana bei yake, Lakini pia hali ya shamba Muda mwingine inapelekea bei kupanda au kushuka.

Baada ya kununua shamba zoezi linalofuata ni kusafisha shamba hilo kwa kukata miti, kung’oa visiki na kuondoa uchafu shambani ili kuwezesha hatua za kupanda na kuhudumia mmea zifanyike katika mazingira rafiki. Gharama za kusafisha shamba kwa ekari moja zinakadiriwa kuwa kati ya laki tano hadi milioni moja (500,000 – 1,000,000/-) Gharama hizi zinategemea na wingi wa miti, hali ya shamba na aina ya teknolojia itakayotumika kusafisha shamba.

NAMNA YA KUMILIKI SHAMBA.
This image has an empty alt attribute; its file name is parachichi-poster.png


Kutokana na Gharama za kununua shamba pamoja na Gharama za kusafisha, kampuni itatoa Gharama ya jumla na ya wastani ambayo itajumuisha Gharama za usafiri, utafiti na ufuatiliaji wa mashamba kwa hatua ya awali; pia kununua na kusafisha shamba hadi kuwa safi. Mwanachama atalipia kiasi cha shillingi milioni moja (1,000,000/-) na kampuni itahakikisha shamba limelipiwa na kusafishwa tayari kwa ajili ya kupanda Parachichi. Hii Gharama ni ya kununua na kusafisha tu ekari moja; Gharama hizi hazijumuishi Gharama za hati, hati itafuatiliwa baada ya kumaliza zoezi la kupanda na mkulima atajulishwa Gharama elekezi za serikali za kulipia hati ya kimila ya kumilikishwa shamba.

Gharama za kununua shamba zitalipwa kwa awamu mbili kama mteja atapenda pia anaweza kulipa mara moja. Awamu ya kwanza italipwa shillingi laki tano ambayo itatumika kwa ajili ya kulipia shamba na gharama za ufuatiliaji ikiwa ni pamoja na usafiri wa timu ya utafiti na miradi. Gharama hizi zitalipwa kupitia akaunti za malipo za kampuni ya JATU kama itakavyoelekezwa kupitia msg inayotumwa katika namba yako ya simu mara tu baada ya kuweka oda kupitia app ya Jatu. Oda za mashamba zimeanza kuwekwa tarehe 07.07.2020 hadi pale tutakapo kamilisha ekari 1000 za awamu ya kwanza. Mkulima au mwanachama ataweka oda ya shamba lake kupitia application ya JATU MARKET inayopatikana Playstore na AppStore.

Awamu ya pili ya laki 5 iliyobaki itaanza kulipwa mwezi ujao kuanzia tarehe 01.08.2020 kwa ajili ya kusafisha mashamba. Hii itatakiwa kulipwa ndani ya mwezi mmoja. Yaani kama mwezi huu umelipia laki 5 ya shamba mwezi ujao lazima ulipie laki 5 nyingine kwa ajili ya usafi wa shamba.

Mtu mmoja anaruhusiwa kumiliki (kununua) kuanzia ekari moja hadi ekari hamsini za kulima Parachichi. Hii ni kwa mujibu wa sheria za ardhi za vijiji Tanzania.

This image has an empty alt attribute; its file name is gettyimages-1136225040.jpg
SEHEMU YA PILI

Shamba la Parachichi linahitaji muda na weledi mkubwa katika maandalizi. Parachichi la kisasa linachukua takribani miezi 36 hadi kuanza kuvuna. Hii ni wastani wa kipindi cha miaka mitatu tangu kupanda. Na baada ya kupata shamba na kulisafisha na kuliweka wazi; hatua zifuatazo ni muhimu katika kupanda na kuhudumia zao la Parachichi.

 1. Kulima shamba lote na kuandaa Mbegu.
  Ekari moja ya shamba ina ukubwa wa mita za mraba 4900. Na kitaalamu tunashauriwa kulima Parachichi kwa kuacha nafasi ya mita saba kutoka mche hadi mche. Hii inapelekea kuwa na jumla ya Miche 100 katika ekar moja. Hata hivyo nafasi hizi za kupanda inategemea na Aina ya mbegu ambayo mkulima atachagua; Kumbuka zipo Aina maarufu zaidi 10 za Parachichi. Jatu tunachagua kulima Aina ya HASS kwa sababu ndiyo mbegu ambayo imethibitisha kufanya vizur katika soko la kimataifa na hata soko la ndani. Pia mbegu hii inavumilia changamoto nyingi za kilimo.
 2. Baada ya kulima shamba tutapiga haro ili kulainisha udongo wote wa shamba na kuchanganya rotuba asilia iliyopo shambani.
 3. Kuchimba mashimo kwa ajili ya kuanza kupanda. Tunatakiwa kuchimba mashimo 100 kwa kila ekar moja.
 4. Kuweka mbolea katika kila Shimo, hapa tutaweka mbolea ya asili kama vile samadi au mboji.
 5. Kupanda miche, kila shimo litapandwa mche mmoja wa Parachichi
 6. Kujenga matuta; kwa kuwa shamba letu lina asili ya mwinuko, na ili kuzuia mmomonyoko wa udongo lazima tujenge matuta katika miche yetu na katika shamba letu kwa kuzingatia kontua.
 7. Kuweka maji ya Umwagiliaji. Kila mmea tutaufungia maji yanayodondoka kila mara ili kuwezesha mti kukua kwa wakati. Hii kitaalamu inaitwa drip irrigation au irrigation sprinkler.
 8. Palizi na huduma ya mmea kila mara. Hili zoezi litaendelea kwa takribani miaka mitatu hadi kuanza kuvuna na inashauriwa usafi uwe mkubwa ili kuzuia wadudu na magonjwa ya mimea. Hivyo kila siku mmea utahudumiwa na wataalamu na kila baada ya miezi mitatu tutafanya palizi kubwa ya shamba zima.
 9. Kupiga dawa, pia hili ni zoez la kila mara wakati wote mmea unapokua
 10. Kupruni, hii pia ni huduma muhimu katika mmea hasa Parachichi ili kuwez kujihakikishia mavuno mazuri msimu ukifika.
 11. Kuanza kuvuna; zoez hili linatarajiwa kuanza baada ya miaka mitatu tangu kupanda. Na hii Ndiyo hatua itakayokamilisha awamu ya kwanza ya mradi huu na baada ya hapa tutaanza kuendesha mradi huu kwa kuzingatia msimu wa kila mwaka. Maana yake gharama za uendeshwaji pia zitapungua sana na zitatolewa kila msimu. Na msimu wa Parachichi ni sawa na mwaka mmoja.
MCHANGANUO WA GHARAMA YA UWEKEZAJI ZAO LA PARACHICHI
This image has an empty alt attribute; its file name is investment-5318530_1920.jpg


Kulingana na hatua tajwa Hapo juu, zifuatazo ni gharama tarajiwa;

GHARAMA YA MWAKA WA KWANZA
———————————————

 1. Kulima mara ya kwanza ~ 60,000/-
 2. Kupiga haro ~ 40,000/-
 3. Kuchimba mashimo na kuweka mbolea @ 5000/- x 100 ~ 500,000/-
 4. Miche na kupanda @ 5000 x 100 ~ 500,000/-
 5. Kujenga matuta @2000 x 100 ~ 200,000/-
 6. Umwagiliaji @ 15,000 x 100 ~ 1,500,000/-
 7. Palizi 4 @ 50,000 x 4 ~ 200,000/-
 8. Dawa ~ 500,000/-
 9. Wataalamu (extensions services) ~ @50,000 kwa mwezi ~ ~600,000/-
 10. Tahadhari ~ 400,000/-

Jumla ya gharama kwa mwaka wa kwanza: 4,500,000/=

GHARAMA YA MWAKA WA PILI
———————————————
Mwaka wa pili matumizi yanapungua na kubaki kama ifuatavyo;

 1. Palizi 4 ~ 50,000 x 4 = 200,000/-
 2. Madawa ~ 500,000/-
 3. Wataalam ~ 600,000/-
 4. Dharura ~ 200,000/-

Jumla ya gharama mwaka wa pili: 1,500,000/=

GHARAMA ZA MWAKA WA TATU
————————————————
Huu mwaka ni mwaka wa mavuno gharama zitaongezeka kidogo kama ifuatavyo ukilinganisha na mwaka wa pili.

 1. Palizi ~ 200,000/-
 2. Madawa ~ 1,000,000/-
 3. Wataalam ~ 500,000/-
 4. Kuvuna ~ 500,000/-
 5. Dharura ~ 400,000/-

Jumla ya gharama kwa mwaka wa tatu: 2,600,000/=

Jumla ya gharama zote kwa miaka mitatu:
4,500,000/ + 1,500,000/ + 2,600,000/ = 8,600,000/=

FAIDA TARAJIWA KWA MAVUNO YA KWANZA YA ZAO LA PARACHICHI:
—————————————————
This image has an empty alt attribute; its file name is hass-avocado-1054729_1920.jpg

Ekari moja yenye miche 100 ya parachichi ikihudumiwa vizur inatarajiwa kutoa matunda kati ya 300 – 500 kwa msimu wa kwanza. Hapa ni wastani wa matunda 400.

Parachichi kawaida inauzwa kwa kupima kwa kilogram. Kwa sasa bei ya parachichi kg 1 kwa soko la njombe inakadiriwa kuwa 1200 – 1500/- na kg 1 inabeba wastani wa matunda ya kawaida NNE (4) na kama matunda yamestawi vizuri Basi Tunda tatu zinafikisha kg 1.

Hivyo Basi wastani wa matunda manne kujaza kg 1 ni sawa na kusema mche mmoja wa matunda 400 unaweza kuzalisha kg 100 Na kwa kuwa bei ya zao hili inazid kupanda; ni dhahiri kwamba kg 1 ya parachichi haiwezi kushuka 1500/- kwa miaka mitatu ijayo. Jatu itaweza kununua kilogram moja kwa bei ya tshs 1500/- au zaidi.

Kama bei itabaki kuwa 1500/- kwa kg maana yake kwa mche mmoja kuna tarajiwa kuwa na kg 100 za parachichi.

1,500/- x 100 = 150,000 mara miche 100 = 15,000,000/- Jumla ya mauzo kwa ekari moja.

Ili kupata faida kwa ekari moja: 15,000,000 – 8,600,000/- =6,400,000/-

Hivyo faida ya kwanza inatarajiwa kuwa milion sita na laki nne.
————————————————

Zao la Parachichi linaweza kuvunwa kwa takribani miaka 30 mfululizo. Ni miaka mitatu tu ya mwanzo ndo kuna gharama kubwa za uendeshwaji. Kwa msimu wa pili na kuendelea faida inatarajiwa kuongezeka kwa sababu mmea utakuwa na uwezo wa kutoa matunda mengi zaidi ukilinganisha na msimu wa kwanza; Lakini pia gharama za uendeshwaji ni ndogo Kwani inakadiriwa kuwa kiasi cha shillingi milion tatu tu kwa msimu na faida inakadiriwa kua zaidi ya milion kumi na tano kwa msimu.

Hili ni zao pekee ambalo mkulima ana uhakika wa kupata zaidi ya tshs 10,000,000/- kila mwaka kama faida isiyo na mashaka.

SEHEMU YA TATU
This image has an empty alt attribute; its file name is whatsapp-image-2020-04-24-at-8.26.59-am.jpeg

Jatu PLC inafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi yake Tanzu inayoitwa JATU SACCOS LTD (JSL).

Jatu imekubaliana na JSL kwamba mkulima wa jatu atapewa mkopo wa kilimo usio kuwa na riba na atalipa deni lake baada ya mavuno.

Kuhusiana na zao hili la kilimo cha Parachichi, mkulima wa jatu atakopeshwa mkopo usio na riba ambao una thamani ya Sawa na 2/3 ya gharama zote kwa ekar moja. Hapa namaanisha gharama za kuhudumia shamba kila mwaka kuanzia mwaka wa kwanza hadi mwaka wa Tatu.

Jumla ya gharama ni shilling milion nane na laki sita, lakin zimegawanyika kila mwaka kwa miaka mitatu.

Kwa mwaka wa kwanza gharama ni milion nne na laki tano, hapa mwanachama anashauriwa kuchangia shiling milion moja na laki tano ambayo ni 1/3 kupitia jatu Saccos. Baada ya kuweka hii 1/3 ~ 1,500,000/- mkulima anaomba mkopo kupitia application ya jatu Saccos Ltd ambayo inajulikana kwa jina la JATU PESA na atakopeshwa shiling milion tatu ili kukamilisha milion nne na laki tano kwa ajili ya kuhudumia shamba lake mwaka wa kwanza. Na hapa tunategemea kuanza rasmi kuanzia January mwaka 2021.

Ifikapo January 2022 mkulima atachangia tena Saccos kwa ajili ya kupata mkopo wa kuhudumia shamba mwaka wa pili. Na hapa jumla ya gharama ni tshs. 1,500,000/- sasa mkulima atachangia laki tano tu ambayo ni 1/3 ya gharama na atakopeshwa shiling milion moja ili kukamilisha gharama zote tshs. 1.5m.

Na ifikapo January 2023 mkulima anatakiwa awe ameweka akiba ya kumuwezesha kupata mkopo wa kuhudumia shamba kwa mwaka wa tatu. Jumla ya gharama kwa mwaka wa tatu ni shiling milion mbili na laki sita (2,600,000). Hapa mkulima atachangia 1/3 jatu Saccos ambayo ni sawa na 867,000/- ili aweze kupata mkopo wa 1,734,000/- .

Mkulima anashauriwa kuwa anaweka akiba kidogo kidogo kila mwezi ili kuweza kupunguza makali ya kuchangia lakin pia kuwezesha akaunt yake kuweza kukopesheka muda wowote Anapohitaji mkopo.

Jatu Saccos Ltd inatoa mkopo usio kuwa na riba kwa wakulima na mkopo huu pamoja na kwamba unaanza kutolewa mwaka 2021, utalipwa kwa pamoja mwaka 2023 baada ya mradi huu kuanza kutoa mavuno ya kwanza.

Kwa kifupi; mkulima wa zao la parachichi atakae Lima kwa mkopo wa jatu Saccos atakuwa amepunguza gharama kwa zaidi ya asilimia 65 ukilinganisha na mkulima anayelima mwenyewe bila jatu. Yaani katika milion nane na laki sita (8,600,000) mkulima anatoa milion mbili na laki nane na kitu (2,866,666/-) ~. Hii pia inamaanisha mwenye uwezo wa kulima ekar moja mwenyewe anaweza kulima ekari 3 akiwa na Jatu.

JATU SACCOS LTD ~ kopa kwa malengo rejesha kwa wakati. Vigezo na masharti kuzingatiwa.

SEHEMU YA NNE

JATU PLC ilianzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kusaidia watanzania kukuza kipato kupitia chakula na kujenga afya zao pia. Ndo maana kirefu cha neno Jatu ni ~ Jenga Afya Tokomeza Umaskini.

Ili kufikia dhima ya JATU, tulikubaliana kujikita katika kilimo, viwanda, masoko na mikopo. Ili kumsaidia mtanzania kutengeneza kipato kupitia chakula cha kila siku, tulilazimika Kuanzisha miradi ya kilimo ili tuweze kuondoa mnyororo wa madalili waliojaa katika biashara ya mazao. Hivyo tukaanza kulima kwa kushirikiana na wanachama wetu. Tunalima ili tufungue viwanda na kuzalisha bidhaa za chakula ambazo tunaziuza kupitia mfumo wetu wa jatu market app.

Hadi sasa tunalima mazao yafuatayo:

 1. Mahindi, kiteto; tunazalisha unga wa mahindi dona na Sembe katika kituo chetu cha kibaigwa, DODOMA.
 2. Alizeti,kiteto; tunazalisha mafuta ya alizet katika kituo chetu cha kibaigwa, DODOMA
 3. Mpunga, kilombero; tunazalisha mchele katika kituo chetu cha kukoboa mpunga kilichopo mbingu kilombero mkoa wa Morogoro.
 4. Maharage, kilindi; tunalima na kufungasha maharage katika kituo chetu cha kilindi mkoani Tanga.
 5. Machungwa, handeni na Muheza; pia tumeanza kilimo cha machungwa katika mkoa wa Tanga kwa lengo la kuzalisha vinywaji na bidhaa zingine zitokanazo na machungwa.

Hivyo Basi, kwa sasa kampuni imeingia katika kilimo cha Parachichi kama
Muendelezo wa mkakati wa jatu kuhakikisha bidhaa zote muhimu zinazoliwa na mwanadamu zinapatikana kupitia mfumo wa jatu na mteja wetu azipate kwa bei nzuri, ziwe na ubora na mteja apate gawio la faida kila mwezi kutokana na manunuzi yake.

Kilimo cha Parachichi mkoa wa Njombe ni mkakati endelevu utakao jumuisha mikoa mingine ya Nyanda za juu kusini na huku tunategemea kujenga kiwanda cha matunda fresh pamoja na kiwanda cha kutengeneza bidhaa mbali mbali zitokanazo na matunda haya. Zao la Parachichi litatuwezesha kutengeneza bidhaa zaidi ya tano ambazo zitauzwa kupitia mfumo wa JATU MARKET APP.

Kampuni inaahidi kwamba itanunua matunda yote ya wakulima wake kwa bei nzuri ya ushindani ili kumwezesha mkulima wake kulima zaidi na kulisha jamii ya jatu kama mkakati unavyosema. Hata hivyo pamoja na kuuza matunda ndani ya Tanzania, kampuni pia imepanga kutumia zao hili na mazao mengine ya matunda kama vile chungwa na apple ambazo tutawaletea Mchanganuo wake hivi Karibuni kuingia katika soko la kidunia. Tutauza matunda nchi mbali mbali duniani na tutavutia wawekezaji zaidi kuja jatu kupitia zao hili.

Mkulima wa jatu atauza matunda ghafi Jatu na Jatu ndo itakayokuwa na mamlaka ya kuchakata au kubrand na kuuza bidhaa hiyo kwa lebo ya kampuni.

JATU – JENGA AFYA TOKOMEZA UMASIKINI

Matukio kwa picha ufuatiliaji wa mashamba ya kilimo cha parachichi Njombe

32 thoughts on “FAHAMU KUHUSU KILIMO CHA PARACHICHI NA JATU MKOANI NJOMBE, PAKUA JATU TALK APP KUPATA TAARIFA ZA MRADI HUU

 1. Safi sasa Mwisho lini kama nahitaji kukodi shamba. Na je kama miko na mashamba mengine yaani maharage na mpunga nikafanikiwa na huku nitakuwa na vigezo vyakupata mkopo iwapo nimekamilisha taratibu za mkopo ama sita ruhusiwa huku labda nisitishe kune kilimo kingine?

  Liked by 1 person

  1. Habari Esther,

   Karibu sana kushiriki huu mradi mwisho wa kubook shamba ni Oktoba mwaka huu pia hata kama upo kwenye mradi mwingine haikuzuhii kupata mkopo kwa mradi huu pia

   Like

 2. Habari samahani nimechelewa kuona post nilikuwa naomba kujua km izzo appricattion za mashamba bado zipo mpk sasa

  Like

 3. Kilimo hiki kinaleta matumaini, Je, mimi niko mkoa wa Shinyanga lakini nafikili kilimo cha parachichi kinaweza kusitawi mikoa ya Geita na kagera, endapo ikiwezekana katika mikoa hiyo je, naweza kuwa mwanachama JATU na kupewa mkopo kwa kuzingatia taratibu na masharti yaliyo wekwa na kama ardhi ya huku hitakubali katika kilimo hiki. Kwetu ni wilaya ya Muleba nyumbani kwangu nimepanda miparachichi kama mitatu naona inastawi vizuri, ispokuwa sijui kwa aina ya mbegu hii mpya aina HASS. Ahsante.

  Like

  1. kupitia kampuni ya JATU PLC unaweza kuwezeshwa mikopo ya maendeleo yenye riba nafuu kwa ajili ya usimamizi wa kilimo chako, asante. Kwa maelezo zaidi tafadhali wasiliana nasi kwa simu namba 0765002660, asante

   Like

   1. Habari naitwa chang’ang’a Niko geita naitaji kuanza kilimo cha parachichi hapa geita naweza kupata muongozo wa khari ya hewa ya mbegu ya kisasa na tabia yake pia maelekezo ya mbolea pia soko liko wapi na je ni uhakika
    Tel:0710780677

    Like

 4. Hallo sir Nina swali kuhusu uwekezaji
  He foreigners wameruhusiwa kuwekeza? Mimi nikifika inchi ya Burundi nahitaji kuwekeza kama kuna utaratibu wowote basi nijulishe.thanks

  Like

 5. Salaam,
  1. Niko Lushoto, je ninaweza kujiunga na JATU na kupata mkopo huo kwa kilimo cha parachichi huku Lushoto Tanga? Je taasisi hii ina ofisi au mwakilishi Tanga, naona huku wanakuja watu kutoka Kenya kununua parachichi hizi kutoka kwa wakulima
  2. Nikiwa huku je naweza kujiunga na JATU nikapata ekari mbili au tatu za kulima parachichi huko Njombe?

  Like

  1. habarI Moses Shemweta, inawezekana kabisa kujiunga na kupata huduma za JATU ikiwemo mikopo na kupata mashamba ukiwa sehemu yoyote. Tafadhali wasiliana nasi kwa simu namba 0758396767 kwa maelezo zaidi. Asante

   Like

 6. Nimeanza kuwasikia juu juu mda mrf kidogo ila sijawahi kupata maelezo ya kina kama haya,nipo interested sana na kilimo hiki na natamani sana nianze uwekezaji katk kilimo nanyi from this year, labda ningependa kujua lini program inaanza kwa mwaka huu?

  Like

 7. Asante sana kwa elimu na ufafanuzi nzuri.
  Ningependa kujiunga ktk mradi huu wa parachichi. Naomba contact

  Like

 8. Mimi naitwa Ng’ango Kalinga,(0629145995)niko mkoa wa IRINGA (IRINGA VIJIJINI)Kijiji cha Ifunda.
  Nimependezwa sana na program yenu ya kilimo cha Parachichi.
  NINA ENEO LA UKUBWA WA EKA 2 ZA MAJI TIRIRIKA TOKA MLIMANI MPAKA PEMBEZONI MWA SHAMBA.
  NAPENDA SANA KULIMA PARACHICHI KUPITIA PROGRAM YENU YA MIKOPO,KUWAPIGIA SIMU NI KUANZIA SANGAPI?

  Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s