FAHAMU KUHUSU JATU PLC- MUUNDO WA KAMPUNI, ENDELEA KUFUATILIA BLOG YETU KWA TAARIFA ZAIDI

Muundo wa Kampuni unajumuisha wanahisa, Bodi ya wakurugenzi, Uongozi wa juu, Wakuu wa idara, Idara, Matawi na wafanyakazi wengine kwenye nafasi tofauti tofauti kama ilivyoelezewa hapo chini:

WASIFU WA WATENDAJI WAKUU

Bw, Peter Isare (29):

Bwana Peter Isare ni mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Kampuni, Amekuwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni tangu kusajiliwa kwa kampuni mwaka 2016.

Bwana Isare ni mhitimu wa shahada ya kwanza ya sheria kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam, hivyo ana taaluma ya sheria na ni mjasiriamali ambaye amejikita kwenye kilimo-biashara. Bwana Peter amedhamiria kubadilisha jamii ya Tanzania, hasa kwa vijana nchini kwa kutumia kilimo kama njia ya kujitengezea kipato.

Wazo la JATU limetokana na mradi ambao ulikuwa chini ya huduma za jamii (asasi isiyo ya kiserikali) iitwayo Legal Protection and Life Improvement Organization (LPLIO) ambayo Peter pia ni mwanzilishi na mwenyekiti.

Taasisi hiyo inashughulika na kulinda haki za binadamu na kuondoa umaskini. Wazo la JATU linaendana na ndoto ya bwana Peter ya kuwa na chombo ambacho kinaweza kuzalisha kipato na kutokomeza umaskini kwa wale ambao wako chini ya piramidi. Kwa nafasi aliyonayo sasa, amekuwa kielelezo cha kuboresha ufanisi wa kiutendaji na kuchochea ukuaji wa Kampuni kwa kuhakikisha kuwa kila mtu ndani ya timu ya JATU anajua jinsi ambavyo jukumu lake ni muhimu kwa mafanikio ya jumla ya Kampuni.

Ana ndoto ya kuwezesha vijana na wakulima wadogo wa Tanzania kusimamia maisha yao kwa faida inayotokana na mnyororo wa thamani unaotokana na kilimo cha pamoja, uchakataji wa mazao, usambazaji na utumiaji wa bidhaa za kilimo kupitia Kampuni.

Bw. Issa Mohamed Simbano (34)

Ni mhitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam na kutunukiwa Shahada ya kwanza ya sheria mnamo mwaka 2016. Pia ni mwanzilishi mwenza wa Kampuni na shirika lisilokua la kiserikali (LPLIO) ambalo lilikuza wazo la JATU kama mradi. Bwana Simbano kwa sasa ni Meneja mkuu wa Kampuni na Katibu wa Bodi ya wakurugenzi. Mnamo mwaka 2015, alikuwa Afisa wa Sheria wa LPLIO.

Alianza uongozi tangu 2012 alipokuwa akisoma Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Ni mtu mwenye msukumo wa kujifunza mwenyewe, mfanyakazi hodari, anayeshirikiana na wengine pia ni mshirika na anaweza kufanya kazi bila kusimamiwa ili kutimiza malengo. Anaendesha dira ya kampuni ya kuwawezesha vijana na wakulima wadogo nchini Tanzania.

Bi. Esther Marino (29)

Esther Marino, ni mwanzilishi wa Kampuni na Mkuu wa Idara ya Fedha. Bi. Esther ana shahada ya masuala ya benki na fedha kutoka Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM) (2012-2015). Hapo awali, alifanya kazi na Kampuni kama Mhasibu kwa muda wa miaka miwili (2) na Wakati huo alionesha uwezo binafsi wa kujihamasisha, ubunifu, na anaweza kufanya kazi chini ya shinikizo. Ana uzoefu mkubwa na wa kuaminika katika Nyanja ya Uhasibu na Fedha ambao alianza kuujenga akiwa kwenye mafunzo ya vitendo katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika wa Serikali ya Tanzania mnamo mwaka 2014.

Bi. Esther Philemon Kiuya (27)

Bi. Esther Philemon ni mmoja wa waanzilishi wa Kampuni na Mkuu wa Idara ya Miradi. Ana Shahada ya kwanza katika Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (2012-2015), Tanzania. Awali, Bi Esther alifanya kazi kama afisa Rasilimali watu wa Kampuni, hivyo ana uzoefu wa miaka mitatu kwenye taaluma hiyo. Kabla ya kujiunga na JATU, alifanya kazi kama Katibu Mkuu wa shirika la (LPLIO) ambalo lilishikilia wazo la JATU kama mradi.

Bi. Mary Richard Chulle (27)

Bi Chulle ni Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Umma, Masoko na Mauzo na pia ni mmoja wa waanzilishi wa Kampuni. Ana uzoefu wa zaidi ya miaka 4 kwenye fani ya masoko. Alipata Shahada yake ya kwanza ya Mahusiano ya Umma na Masoko katika Chuo Kikuu cha St. Augustine mnamo mwaka 2015.

Uzoefu wa Bi Chulle umetokana na kufanya kazi kwenye taasisi mbalimbali ikiwemo Sunda International ambapo alifanya kazi kama Afisa wa Huduma kwa Wateja na mauzo mnamo mwaka 2017 hadi 2018; Maria stopes Tanzania ambapo alifanya kazi kama karani wa data kuanzia 2016 hadi 2017 na Pia Kifaru Community Development Tanzania ambapo alifanya kazi kama afisa Miradi kanzia 2014 hadi 2016 na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ambapo alifanya kazi kama na Afisa mahusiano ya Umma na Masoko mnamo mwaka 2014

Bw. Moses Lukoo William (27)

Bw. Lukoo, ni mmoja wa Waanzilishi wa Kampuni na Mkuu kwa idara ya TEHAMA. Alihitimu Stashahada katika Teknohama kutoka St Joseph Instutute of Business and Management, Morogoro Tanzania ambapo alikuwa mwanafunzi bora kabisa katika mwaka wake wa mwisho 2015/2016. Ana uzoefu wa miaka mitatu wa kufanya kazi na ana utaalam mkubwa katika kusimamia mifumo ya teknolojia ya mawasiliano. Bw. Lukoo ni mbobezi kwenye Usimamizi wa Mifumo ya mtandao, kutatua matatizo ya kimtandao , kutunza na kutengeneza vifaa vya kompyuta na ubunifu wa picha. Pia ni mzoefu kwenye utoaji wa mafunzo na kujenga uwezo wa matumizi ya mifumo ya mtandaoni.

Bw. Paul Kapalata (36)

Bw. Paul Kapalata ni Mkuu wa Idara ya Utafiti na mwanzilishi mwenza wa kampuni. Alikuwa Mkuu wa Idara ya Miradi ya Kilimo tangu 2016 hadi 2018 kwenye Kampuni. Alihitimu Shahada ya kwanza kwenye masuala ya Benki na fedha kutoka Chuo Kikuu cha Kampala cha jijini Dar es salaam (2010-2013).

Pia, ana cheti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mchele ya Kimataifa ya Manilla Ufilipino (2019). Kabla ya kujiunga na Kampuni, Bw. Paul alifanya kazi kama afisa mtendaji wa ukuzaji biashara wa TTES CO. LTD (2012); kama Afisa Masoko wa Tanjap Empex (2010-2011) na mshauri wa wateja katika Benki ya Barclays Tanzania (2008-2010).

Bw. Kenneth John Maganga (29)

Kenneth John Maganga ni Mkuu wa Idara ya Uzalishaji, Usafirishaji na Usambazaji wa bidhaa na pia ni mmoja wa waanzilishi wa Kampuni. Ana uzoefu katika utangazaji wa redio, uandishi wa habari na mahusiano ya Umma. Awali alikuwa mkuu wa Idara ya mauzo na Meneja Uzalishaji wa Tawi la Kibaigwa (2018-2019).

Ana diploma ya uandishi wa habari kutoka Shule ya Uandishi wa Habari ya Dar es salaam (DSJ) (2011-2013). Kenneth amefanya kazi kama Afisa Mahusiano ya Umma, Mtangazaji wa Redio na Mhariri wa Habari katika vyombo tofauti vya habari nchini Tanzania kama WAPO RADIO ambapo alikuwa Mwandishi wa Habari (2011 – 2012) na RADIO TUMAINI kama Mtangazaji wa vipindi vya watoto (2012-2013).

Bi. Rebecca Kashindye Joseph (24)

Bi. Rebecca Kashindye Joseph ni Mkuu wa Idara ya Rasilimali watu na Sheria. Ana Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Mwanza. Kabla ya kujiunga na Kampuni Bi. Rebecca alifanya kazi kama Msimamizi Msaidizi katika kampuni ya forever Living Na Afisa habari na Masoko katika shirika la Her-Inititiative, asasi isiyo ya kiserikali ambayo inashughulika juu ya kuwawezesha na kuwasaidia wasichana wadogo kupitia mafunzo ya ujasiriamali nchini Tanzania (2015-2019).

MUHTASARI WA WASIFU WA BODI YA WAKURUGENZI

Mhandisi Dk. Zaipuna Obedi Yonah (60)

Mhandisi. Dk Zaipuna Obedi Yonah aliteuliwa kuwa mjumbe na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi mnamo Juni 2019. Ana shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa umeme kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es salaam (1985), Shahada ya uzamili (1988) na shahada ya uzamivu Ph. D. (1994) katika Uhandisi wa Umeme kutoka Chuo Kikuu cha Saskatchewan, Saskatoon – Canada.

Yeye ni Mhandisi Mshauri katika Mawasiliano aliyesajiliwa. Amebobea katika utengenezaji/uongezaji wa thamani, uwezeshaji na ulinzi kupitia Teknohama, na ana uwezo ambao unaweza kutumika kwenye kilimo, usindikaji na uchakataji wa vyakula, usambazaji wabidhaa, mahitaji ya bidhaa na matumizi ya bidhaa za kilimo.

Ni Mkurugenzi Mtendaji na Mshauri Mwandamizi katika kampuni ya Applied Engineer-ing & Byte-Works(T) Limited (AEBW), Kampuni ya uhandisi wa Teknohama na Mawasiliano ya simu. Pia ni Mtafiti Mwandamizi katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ya Afrika (NMAIST) na Mwanachama wa IEEE Inc. Ana zaidi ya miaka 35 ya kufanya kazi katika Nyanja tofauti kama vile nafasi za umeneja na kuunda mikakati na maendeleo ya biashara (Chuo Kikuu cha Dar es salaam – 1985- 2000, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ya Afrika (NM-AIST) mwaka 2013 hadi sasa, (Mkurugenzi wa Taarifa za Mitandao na ubunifu wa bidhaa kwenye shirika la TTCL 1998 – 2008) na utengenezaji wa sera katika Teknohama Sekta za Mawasiliano ya simu Mkurugenzi wa Teknohama Serikalini) na kazi zingine ndani ya Tanzania (Alileta mapinduzi ya mkongo wa taifa wa Mawasiliano (NICTBB): 2008 – 2013) kwenye jumuiya za Afrika Mashariki na SADC.

Kwenye Kampuni ameleta uzoefu alioupata kwenye kuunda na kuongoza timu zenye utendaji kazi mkubwa kwa uadilifu na mapendekezo yenye tija hivyo kufikia malengo ya kampuni. Ana uzoefu katika kutoa mafunzo, utafiti, uandaaji na utekelezaji wa miradi, kutoa ushauri na kuunda timu, na kutumia tafiti za kisayansi na teknohama kwenye uzalishaji na fikra jumuishi ili kuwawezesha watu kuondokana na umaskini. Hivyo basi ni aina ya mtu ambaye anajitolea na kuwa kiongozi bora.

Bw. Abdallah Gonzi (44)

Abdallah Gonzi ana Shahada ya Sheria (2004) na shahada ya Uzamili ya Sheria (2006) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es sa-laam. Katika shahada yake ya uzamili alijikita katika Uongozi wa Mashirika. Kwa sasa ni mtahiniwa wa shahada ya uzamivu katika sheria. Bwana Gonzi ni wakili na mhadhiri katika shule ya sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Analeta uzoefu wake mkubwa alionao kwenye sheria na uongozi katika kampuni.

Kitaaluma amejikita sana kwenye sheria za biashara, usuluhishi wa kimataifa, usuluhishi, haki za binadamu, sheria za mwenendo wa kesi za madai pamoja na sheria za jinai.

Bi. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda (42)

Emmanuela Mtatifikolo Kaganda ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ambayo ilithibitishwa na Mkutano Mkuu mnamo Juni 2019. Bi. Kaganda aliteuliwa kwenye bodi kutokana na uzoefu wake kwenye taaluma za afya ya jamii, mawasiliano ya umma na mahusiano ya jamii, uhusiano wa Kimataifa, dhana ya miradi ya jamii, ubunifu, utekelezaji na usimamizi wake, pia uhamasishaji wa jamii na kuthaminisha bidhaa.

Ana shahada ya Mawasiliano ya habari kutoka chuo kikuu cha Mt. Augustino Mwanza (2004) na Shahada ya uzamili kwenye afya ya jamii kutoka chuo kikuu cha Afya ya Jamii cha Jiji la New York (CUNY) (2017) Bi. Kaganda amepata uzoefu wake kwa kufanya kazi kama Mkurugenzi wa Vijana Malezi Initiatives (VMI) (2017 hadi sasa), kama mratibu wa ujenzi na uanzishaji wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere (MJNLS) (2017 hadi leo); kama Mjumbe wa Bodi ya SEWOTA (2017 hadi sasa), na kama Mratibu wa miradi, haswa Miradi ya Vijana, Kanda ya Afrika chini ya United Evangelical Mission (UEM)

Bi. Mwajuma Hamza (31)

Bi.Mwajuma Hamza aliteuliwa kuwa Mjumbe na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Kampuni mnamo juni 2019. Uteuzi wake ulitokana na sifa inayohusishwa na uzoefu wake mkubwa katika kukuza biashara na utaalam wa uhamasishaji jamii. Ana shahada ya uzamili ya Biashara ya Kimataifa (MIT) kutoka shule ya Biashara (UDBS) na Shahada katika Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam. Bi Hamza ni mtaalam wa biashara na ujasiriamali kutoka Tanzania na ana uzoefu wa miaka sita kwenye fani hiyo.

Kwa sasa anafanya kazi na chama cha wanawake wafanyabiashara (TWCC) kama Mkurugenzi Mtendaji wa muda. Pia ni mtaalam wa uwezeshaji wanawake kwenye masuala ya kiuchumi kama vile kukuza biashara, ujasiriamali, manunuzi, maendeleo ya biashara na masoko, ni Mchambuzi wa sera na mkufunzi wa biashara za kimataifa. Alihudhuria mafunzo kadhaa ikiwa ni pamoja na uongozi, Ujuzi wa ushindani, mauzo ya nje, jukumu la taasisi inayounga mkono biashara, Ubora na viwango, upangaji wa miradi na usimamizi, Utetezi, ustadi wa maonyesho, biashara ufadhili na biashara ya nje ya mipaka ya nchi. Amefanikiwa kuanzisha miradi kadhaa na mipango ya uwezeshaji wanawake na vijana kiuchumi na kusaidia vijana wengi na vikundi vya wanawake kwa kutoa mafunzo. Yeye pia ni mwanachama wa vyama na Kamati kadhaa za Kitaifa na kibiashara. Mwajuma pia ni mkufunzi na Mshauri wa mashirika tofauti ya Vijana nchini na ni mwanaharakati wa vijana kujiajiri. Katika kampuni ya JATU anaongeza utaalam wake katika biashara na usimamizi wa programu za kusaidia kufanikisha maono ya Kampuni.

Bw. Phinias Opanga (48)

Bwana Phinias Opanga aliteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni mnamo Juni, 2019. Opanga ana Stashahada ya Juu ya Uhasibu kutoka Taasisi ya Usimamizi wa Fedha, (IFM) Tanzania (1999), Stashahada ya Uzamili ya Uhasibu kutoka Taasisi ya Uhasibu Arusha (2011), na ni mhasibu wa umma aliyethibitishwa (CPA(T) (2012). Yeye pia ni mkaguzi wa Hesabu za Umma aliyethibitishwa (ACPA) na Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi ya Taifa (NBAA), Tanzania.

Ni mzoefu katika kuandaa kanuni za kifedha na sera za uhasibu, uboreshaji wa Mifumo ya habari ya Uhasibu, kubuni mifumo ya Udhibiti wa ndani, utayarishaji wa sera zilizojumuishwa na zisizo za upeanaji, utayarishaji wa pamoja na taarifa zisizojumuishwa za kifedha, utayarishaji wa Vitabu vya Uhasibu, kuwa mjumbe wa bodi ya Zabuni, ni hodari katika kupanga bajeti na usimamizi vihatarishi na majanga na kutumia Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (misingi ya IPSAS). Alipata uzoefu wake wa kina kwenye Uhasibu kutokana na kufanya kazi za uhasibu na mienendo ya usimamizi wa kifedha huko Mansoor Daya & Co Ltd (2000 – 2003); Faulu Tanzania Limited (2003); Wizara ya Fedha na Mipango ya Tanzania (2006 – 2014); kama Mhasibu Mwandamizi katika Idara ya Umwagiliaji wa Wizara ya Kilimo na Usalama wa Chakula (2014 – 2016); kama Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala na Mamlaka ya Maendeleo ya Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) (Aprili 2015 – 2016). Kwa sasa anafanya kazi kama Mhasibu Mwandamizi anayesimamia Kitengo cha Fedha na Wakala wa Taifa wa utafiti wa Nyumba na majengo (Julai 2016 hadi leo).

Katika kampuni ya JATU anaongeza uzoefu mkubwa wa zaidi ya miaka 19 ya utekelezaji wa Mifumo ya habari ya Uhasibu. ustadi wa usimamizi wa vihatarishi na majanga, uchambuzi wa taarifa za kifedha na kutoa ushauri mkubwa katika maamuzi sahihi ya kifedha.

Bw. Ian Semakande (43)

Bw. Ian Samakande aliteuliwa na kuthibitishwa kuwa mjumbe wa Bodi Ya Kampuni mnamo Juni 2019. Uteuzi wake ulitokana na utendaji wake madhubuti na wenye kushawishi katika Uhandisi wa Kilimo, haswa katika nyanja za upangaji, Ubunifu na usanifu wa mitambo ya shamba, umwagiliaji, utunzaji mazao na usindikaji.

Ana Shahada ya Sayansi katika Uhandisi Kilimo Kutoka Chuo Kikuu cha Zimbabwe (2000). Uzoefu wa Samakande umejengwa tangu mwaka 2000 kutokana na Utendaji wa mifumo ya umwagiliaji na usimamizi wa matumizi ya maji wakati akifanya kazi na Chuo Kikuu cha Zimbabwe (2000 – 2003); kama mhandisi mtafiti na Kituo cha Teknolojia ya Umwagiliaji cha Zimbabwe, kitengo cha Kituo cha Teknolojia ya Umwagiliaji cha Zimbabwe, kitengo cha Wizara ya Kilimo cha Zimbabwe (2004 -2008). Katika kipindi hicho, aliendeleza na kuainisha ujuzi wake wa vifaa vya kupima umwagiliaji (vilivyoingizwa au kutengenezwa ndani ya nchi) na kuanzisha mashamba ya mfano na kufufua mifumo ya umwagiliaji ikiwa ni pamoja na mfumo wa matone, kumwagilia na pivot.

Mnamo mwaka 2008, alianzisha Irrigrow Global Ltd, Kampuni binafsi ya umwagiliaji nchini Tanzania ambayo ililenga katika kubuni na ufungaji wa mifumo ya umwagiliaji, usanikishaji wa viboreshaji vya bustani, kubuni na ujenzi wa mifumo ya uhifadhi wa maji shambani na ugavi na ufungaji wa mifumo ya kusukuma jua; mfano mzuri ni mradi wa maendeleo ulioko huko Iringa ukijumuisha matone na mifumo ya kusukuma maji ya jua huko Igingilanyi, Wangama na Tanangozi. Wateja wa Mhandisi Samakande ni pamoja na watu binafsi na miradi ya maendeleo inayohitaji mifumo ya umwagiliaji wa matone ambayo yanalenga katika kuongeza matumizi ya maji wakati wa kuongeza uzalishaji.

Bw. Samakande analeta katika Kampuni uzoefu wa zaidi ya miaka 10 ya harakati za kufanya bidhaa za shamba na kilimo ziwe za kibiashara. Uzoefu na ujuzi alionao ili kutumiwa kuanzisha mashamba mazuri na kuongeza uzalishaji kutoka kwenye mashamba ya Kampuni.

NENO KUTOKA KWA MKURUGENZI

Ndugu Wawekezaji,

Kwa niaba ya uongozi na wafanyakazi wa JATU. Nawakaribisha kuwekeza JATU. Tunafurahi kuona mmeamua kutaka kuwekeza katika kampuni yetu. JATU inamilikiwa zaidi na vijana na wakulima wadogo wadogo nchini. Dira ya kampuni ya JATU ni kuwa kampuni inayoongoza kwa kutoa huduma bora kwa wateja ndani na nje ya nchi katika kilimo biashara na bidhaa za kilimo na kutoa faida nzuri kwa wawekezaji wa kampuni.

Kwa kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwa kampuni mwaka 2016. Kampuni imeweza kuunganisha mamia ya wakulima wadogo wadogo katika maeneo mbalimbali hapa nchini kupitia kilimo cha kisasa na usimamizi. Shughuli za kilimo na uchakataji wa mazao zilianzishwa katika mikoa ya Morogoro, Tanga, Dodoma na Manyara. Kwa siku zijazo tunatarajia kuanzisha vilimo kama hivi katika mikoa mingine hapa Tanzania. Kwa upande wa huduma maelfu ya wateja wetu wamejiunga na kampuni na wanafurahia huduma zetu bora katika maeneo mbalimbali hapa nchini ambazo ofisi zetu zinapatikana kama vile ofisi ya Mtwara iliyopo kanda ya kusini,ofisi ya Arusha iliyopo kanda ya kasikazini, ofisi ya Mwanza iliyopo kanda ya ziwa na makao makuu ya kampuni yalipo mkoa wa Dar es Salaam. Vile vile tuna matawi mengine yaliyopo sehemu za uzalishaji ambapo tunaendesha shughuli za kilimo na uchakataji wa bidhaa kama vile Kibaigwa – Dodoma kwa kuchakata unga wa mahindi na kukamua alizeti, Mbingu – Morogoro kiwanda cha kumenya mchele, Kiteto – Manyara na Kilindi – Tanga kwa kilimo cha mahindi, alizeti na Maharage.

Lengo letu ni kufikia wilaya zote nchini na kutoa huduma za kilimo, viwanda na masoko. Kampuni inatazamia kuleta matokeo chanya katika jamii ya Tanzania na zaidi kupitia kilimo, vi-wanda, huduma za kifedha (mikopo) na masoko. Tunashukuru mpango mkakati wetu wa masoko ambao unahusisha kuwalipa wateja wetu gawio kila mwezi kutokana na manunuzi yao ya kila siku. Kampuni inazidi kufanikiwa kupata wateja na kukuza soko lake pamoja na kuwa chaguo bora kwa jamii katika uwekezaji na usambazaji wa bidhaa za kilimo kwaajili ya matumizi ya kila siku. Kwa njia hii ya kupunguza umasikini, mda umefika wa kampuni kuamia katika umiliki wa umma, maono haya yakichukuliwa hatua muhimu yataleta faida kubwa kwa wawekezaji wetu wa sasa na wa baadaye, wafanyakazi wetu na wateja wetu. Tunauhakika kwamba uthubutu na ubunifu ulioijenga JATU kuwa kampuni bora ya kilimo biashara utaendelea kujenga malengo yake ya kuwa kampuni ya umma.

Natazamia mahusiano ya muda mrefu na yenye mafanikio ya pamoja, na nyinyi wawekezaji wetu wapya.

PETER ISARE

MKURUGENZI MTENDAJI JATU PLC

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s